Polisi nchini kenya wanachunguza kifo cha polisi james mugo kabachia aliyefariki baada ya bastola aliyokuwa ameishika kudaiwa kutoa risasi

Polisi Nchini Kenya wanachunguza hali ya sintofahamu kuhusu Afisa Mkuu wa Polisi aitwaye James Mugo Kabachia aliyefariki baada ya bastola aliyokuwa ameishika kudaiwa kutoa risasi iliyomuua katika kituo cha Polisi cha Kegonga, Kuria, kaunti ya Migori, Kenya.

Kabachia ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Kuria mashariki alipoteza damu nyingi kufuatia jeraha alilopata jana July 01,2024 jioni kutokana na tukio hilo na kupelekea kifo chake, Vyombo vya Habari vya Kenya vimeripoti.

Tukio hilo lilitokea saa kumi jioni ya jana alipokuwa akipokea silaha hiyo kwa shughuli za usiku, Polisi wamesema alikuwa akipokea bastola kutoka katika ghala la silaha la kituo na alikuwa akichukua tahadhari za usalama kwenye silaha hiyo ambayo ilifyetuka na risasi kumjeruhi vibaya.

Afisa ambaye anasimamia ghala hilo la silaha aliripoti kuwa alimpatia Mugo bastola aina ya Berreta iliyokuwa na risasi 15 lakini mambo yalibadilika alipoamua kufanya ukaguzi wa usalama kwenye silaha hiyo, ukaguzi wa tahadhari ni wa kawaida na muhimu kwa Wamiliki, kuwa na uhakika wa usalama wa silaha lakini jinsi tahadhari zinavyofanywa zinaweza kugeuka kuwa mbaya, hapo ndipo aliporipotiwa kutoa risasi moja kutoka kwenye silaha iliyojigonga kwenye sehemu ya paja la kulia.

Mwili wa Marehemu ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri kufanyiwa uchunguzi, Polisi wamesema wanakusudia kuchunguza jinsi tukio hilo lilivyotokea, Mashuhuda wa tukio na waliotoa maelezo ya awali ni miongoni mwa watakaohojiwa kuhusu tukio hilo.

Share: