Papua new guinea: zaidi ya watu 2,000 wamefukiwa katika maporomoko makubwa ya ardhi yaliyosomba kijiji kimoja

Papua New Guinea imeifahamisha Umoja wa Mataifa kwamba zaidi ya watu 2,000 wamefukiwa katika maporomoko makubwa ya ardhi yaliyosomba kijiji kimoja, kulingana na nakala ya barua hiyo iliyopatikana na Shirika la Habari la AFP.

“Maporomoko ya ardhi yalizika zaidi ya watu 2,000 wakiwa hai na kusababisha uharibifu mkubwa,” kituo cha kitaifa cha maafa nchini humo kiliiambia ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu Port Moresby.


Kijiji cha mlimani kilichokuwa na shughuli nyingi katika mkoa wa Enga kilikaribia kuangamizwa wakati kipande cha Mlima Mungalo kiliporomoka alfajiri ya Ijumaa, na kuzika nyumba nyingi na watu waliokuwa wamelala ndani humo.

Maporomoko hayo ya ardhi yalisababisha “uharibifu mkubwa kwa majengo, mashamba ya vyakula na kusababisha athari kubwa katika maisha ya kiuchumi ya nchi,” ofisi ya maafa ilisema.


Barabara kuu ya kuelekea Mgodi wa Porgera “ilikuwa imefungwa kabisa,” ilisema sehemu ya barua hiyo, ambayo ilipokelewa na maafisa wa Umoja wa Mataifa Jumatatu asubuhi.

Takriban watu 1,250 wamekimbia makazi yao huku zaidi ya nyumba 150 zikifukiwa na takriban nyumba 250 zilitelekezwa.

Share: