Papa Francis afariki akiwa na umri wa miaka 88, Vatican inasema

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis alifariki dunia Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88 katika makazi yake katika Casa Santa Marta, Vatican.

Muda mfupi uliopita, Mwadhama, Kardinali Farrell, alitangaza kwa masikitiko kifo cha Baba Mtakatifu Francis, kwa maneno haya:

"Ndugu wapendwa, kwa huzuni kubwa sina budi kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francisko''.

Saa 7:35 asubuhi ya leo (saa za huko), Askofu wa Roma, Francis, alirudi nyumbani kwa Baba. Maisha yake yote yaliwekwa wakfu kwa huduma ya Bwana na Kanisa Lake."

"Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo wa ulimwengu wote, hasa kwa ajili ya maskini zaidi na waliotengwa zaidi."

Farrell anaongeza: "Kwa shukrani nyingi sana kwa ajili ya kielelezo chake kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunaipongeza roho ya Papa Francisko kwa upendo wa huruma usio na kikomo wa Mungu Mmoja na wa Utatu."

Kifo cha Papa kimekuja chini ya saa 24 baada ya kujitokeza kwenye Uwanja wa St Peter's Square mjini Vatican kwa ajili ya Jumapili ya Pasaka.

Alitoka akiwa kwenye kiti cha magurudumu na kupunga mkono kutoka kwenye baraza ya Basilica ya St Peter's kwa umati wa watu waliokuwa wakishangilia na kusema: "Ndugu wapendwa, Pasaka njema."

Hotuba yake ya Pasaka na baraka ilisomwa na msaidizi alipokuwa ameketi, akitazama.

Baada ya baraka, alizungushwa kwenye uwanja. Alipopita katikati ya umati, msafara wake ulisimama mara kadhaa huku watoto wachanga wakiletwa ili awabariki.


Ikulu ya White House imetoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Papa katika chapisho kwenye mtandao wa X.

"Pumzika kwa Amani, Papa Francis," chapisho hilo linasema, pamoja na picha ya Papa akikutana na Rais wa Marekani Donald Trump na mkewe Melania, na picha nyingine ya Papa akikutana na JD Vance jana.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen anasema "aliongoza mamilioni, mbali zaidi ya Kanisa Katoliki, kwa unyenyekevu na upendo wake safi kwa wasiojiweza"

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi anasema "ameumizwa sana" na kifo cha Papa Francis.

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk anamkumbuka Papa Francis kama "mtu mzuri na mchangamfu "

Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi anasema Papa Francis "alikuwa sauti ya amani, upendo na huruma"

Share: