Nigeria: mahakama imemhukumu kifo mfanyabiashara wa china kwa kumuua mpenzi wake

Mahakama nchini Nigeria imemhukumu kifo mfanyabiashara wa China baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mpenzi wake Ummu Kulthum Sani mwaka 2022.

Frank Geng Quarong alipatikana katika chumba chake baada ya kumchoma kisu mara kadhaa.

Mauaji ya mwanafunzi huyo wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 22 yalishtua Wanigeria na tukio hilo likafuatiliwa kwa karibu.

Hukumu za kifo ni nadra nchini Nigeria. Quarong ana siku 90 za kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya familia, kaka wa mwathiriwa, Sadiq Sani, alielezea hukumu ya kifo kwa kunyongwa iliyotolewa na mahakama ya Kano kuwa ni haki. Alisema kuwa yeyote anayemuua yeyote anastahili kuuawa pia.

"Tunamshukuru Mungu kwa kutuonyesha siku hii... Naomba kwamba roho ya dada yangu iendelee kupumzika kwa amani," 

Familia yake inamkumbuka mwanafunzi huyo mchanga wa kilimo kama mkarimu na mcheshi.

Quarong, 49, na Bi Sani walikuwa kwenye uhusiano tangu 2020 baada ya kukutana katika duka kubwa, kulingana na Bw Sani.

Jamaa huyo alikuwa nchini humo akifanya kazi katika kampuni ya nguo ya Nigeria.

Akiongea muda mfupi baada ya mauaji hayo mnamo Septemba 2022, rafiki wa familia Ahmad Abdullahi alielezea kilichotokea.

Alikumbuka kuja nyumbani kwa familia na kuona kwamba "watu wengi walikuwa wamekusanyika nje ya nyumba".

"Hapo ndipo tulipojua kuwa kuna jambo baya limetokea. Geng alikuwa mpenzi wake na alikuwa na mahusiano mazuri na familia yake kabla ya siku hiyo.

"Kabla ya tukio walikuwa na matatizo kwani hakuwa na mapenzi naye tena naye Geng hakutaka kuachilia."

Kulingana na majirani, usiku wa mauaji hayo Quarong alisikika akigonga sana lango mlango wa nyumba ya familia ya Sani.

Mama yake Sani alipofungua geti alimsogeza pembeni na kukimbilia moja kwa moja chumbani kwake huku akifunga kwa ndani.

Kelele na vilio vyake viliivutia familia hiyo na kabla ya mtu yeyote kuvunja mlango kumsaidia alikuwa amedungwa kisu mara kadhaa.

Alikufa baadaye hospitalini.

Kwa sasa Nigeria ina zaidi ya watu 3,400 wanaosubiri kunyongwa na mara ya mwisho kunyongwa kulifanyika mwaka 2012.

Share: