Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha kutokea kwa tukio la mauaji ya kusikitisha lililomhusisha Stephano Evaristo Mwambeje (23), mkazi wa Chapwa “A” Wilaya ya Momba. Tukio hili limetokea usiku wa Novemba 26, 2024, majira ya saa 4:30, katika mtaa wa Chapwa “A”.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 27, 2024, na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, SACP Augustino Senga, marehemu Mwambeje alivamiwa na watu wasiojulikana wakiwa nyumbani kwake akiwa amelala. Wavamizi hao walivunja mlango wa nyumba yake na kumshambulia kwa vitu vyenye makali kichwani na mikononi, hali iliyosababisha kifo chake.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata mtu mmoja, dereva bodaboda, kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo. Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio na wahusika wengine waliopanga na kutekeleza mauaji haya.
Kamanda Senga pia ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuhusika katika matukio ya kihalifu, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahalifu wote.