Mtanzania abraham mgowano aripotiwa kupoteza maisha baada ya kutumbukia kwenye mto miami marekani

Mwili wa Abraham Mgowano (35) ambaye 7news ya Marekani imeripoti kuwa ni Mtanzania, umekutwa ukielea kwenye Mto Miami katika Jimbo la Florida Nchini Marekani ikiwa ni baada ya Mwanaume huyo kuripotiwa kuanguka kutoka kwenye boti.

Taarifa imeeleza kuwa Polisi walipokea simu ya Mtu kutoka eneo la tukio akisema ameona mwili ukiwa unaelea mtoni siku ya Jumanne February 27 ikiwa ni siku tatu toka Mgowano aripotiwe kuanguka kutoka kwenye Boti siku ya Jumamosi saa mbili na nusu usiku.

Imeelezwa kuwa siku ya tukio, Mgowano alikua na Watu wengine kumi na tatu kwenye Boti hiyo akiwemo anayeendesha ambapo muda mfupi tu baada ya kupokea taarifa za kuanguka kwake Vikosi vya uokoaji vikiwemo vya Polisi, Vikosi vya Ulinzi wa Pwani na Wazamiaji walianza kumsaka lakini hawakufanikiwa.

Taarifa ya Polisi imesema Mgowano alikwenda Miami kwa ajili ya kutalii akitokea Mji wa Berkeley uliopo Kaskazini mwa Jimbo la California ambapo akaunti zake za mitandao ya kijamii zimeonesha kuwa alikua akifanya kazi kama Injinia katika Kampuni ya Google ( software engineer).

Kwa mujibu wa taarifa, Abraham alikuwa Mfanyakazi wa Google kwa miaka 9 baada ya kuwa mmoja wa Wanafunzi bora kutoka Chuo Kikuu cha Stanford. Baadaye aliajiriwa kama Mshauri wa Masuala ya Kompyuta chuoni hapo kwa mwaka mmoja

Aidha, Mtanzania huyo alikuwa kati ya Wanafunzi Bora 12 waliofaulu vizuri Mtihani wa Kidato cha 4 mwaka 2007 ambapo walipata nafasi ya kukutana na kupongezwa na Rais Jakaya Kikwete

Share: