Mombasa: mahakama ya shanzu imeipa ofisi ya mkuu wa mashtaka ya umma dpp siku 14 dhidi ya paul makenzi

Mackenzie na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka takriban 12, yakiwemo ugaidi, mauaji, kusaidia kujitoa uhai, utekaji nyara, itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, ulaghai na utakatishaji fedha.

Mahakama ya Shanzu mjini Mombasa Pwani ya Kenya, imeipa Ofisi ya Mkuu Wa Mashtaka Ya Umma - DPP siku 14, kumfungulia mashtaka mshukiwa mkuu wa mauaji ya watu huko Shakahola mchungaji mwenye utata, Paul Makenzi na wafuasi wake 29 la sivyo imuachilie huru.

Akitoa agizo hilo, Hakimu Mkuu Mwandamizi katika mahakama ya Shanzu Yusuf Shikanda, amesema ombi la afisa msaidizi kutoka ofisi ya DPP Jami Yamina la kutaka kumzuilia Mackenzie kwa siku 180 ili kuruhusu wapelelezi kuhitimisha uchunguzi wao, "limepitwa na wakati."

Hakimu Shikanda alisema kuwa washukiwa hao wamesalia rumande kwa siku 117 tangu maombi hayo kutoka ofisi ya mashtaka ya umma yawasilishwe tarehe 18 Septemba mwaka 2023.

Aliongeza kuwa kesi hiyo haikusikizwa mara moja baada ya kuwakilishwa mahakamani kwa sababu ya mambo yaliyoingilia kati na uamuzi huo pia ulilazimika kucheleweshwa kwa sababu zisizoepukika.

Mackenzie na watuhumiwa wenzake wamekaa rumande kwa zaidi ya miezi mitatu tangu kuwasilishwa kwa maombi ya kuongezewa muda wa kumzuilia.

Mahakama ilisema muda huo unatosha kwa wapelelezi kukamilisha uchunguzi wao ili kutoa nafasi kwa ofisi ya DPP kufanya uamuzi wa kuanza mashtaka.

“Iwapo hakuna uamuzi wa kuwafungulia mashtaka walalamikiwa baada ya kumalizika kwa muda huo, mahakama itazingatia kuwaachia huru walalamikiwa kwa masharti yatakayoamuliwa na mahakama,'' alisema hakimu huyo.

Kesi hiyo itatajwa tarehe 23 Januari 2024 kwa maagizo zaidi.

Mackenzie kwa mara ya kwanza alikamatwa April 15 mwaka 2023 akituhumiwa kuwashawishi wafuasi wake wa kanisa la Good News International eneo la Malindi katika msitu wa Shakahola, kufunga kula wakiwa na matumaini ya 'kumuona Yesu Kristo.'

Mackenzie na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka takriban 12, yakiwemo ugaidi, mauaji, kusaidia kujitoa uhai, utekaji nyara, itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, ulaghai na utakatishaji fedha.

Zaidi ya wafuasi 425 walifariki wengi wao wakiwa watoto na wanawake.

Share: