Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Daniel Changolo, amesema kuwa mkoa wa Songwe unaweza kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania, na viongozi wa serikali tayari wameanza juhudi za kuweka mipango thabiti kufanikisha jambo hilo.
Mh.Chongolo amesema hayo wakati akipokea vifaa vya michezo kutoka kwa Benki ya Tanzania Commercial Bank (TCB), Mheshimiwa Changolo alieleza kuwa wamekutana na Chama cha Mpira wa Miguu Songwe (SOREFA) ili kuandaa mikakati ya kufanikisha lengo hilo.
Benki ya Tanzania Commercial Bank imetoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 17.5, ikiwa ni mchango wao katika kuunga mkono na kuendeleza michezo mkoani Songwe. Songwe ni miongoni mwa mikoa ambayo haina timu katika madaraja ya juu ukilinganisha na mikoa mingine nchini Tanzania.
Mheshimiwa Changolo ameonyesha matumaini kuwa msaada huu wa vifaa utachangia katika kuimarisha mazingira ya michezo mkoani na kuleta hamasa zaidi kwa timu za mkoa wa Songwe.