Mhe. kapinga: hatutawavumilia wasambazaji wa vifaa vya umeme walio wazembe

kama unafanya uzembe kwa kuwapa kazi na mikataba wasambazaji ambao hawana uwezo au wanaoshindwa kufanya kazi na hamuwachukulii hatua tutaanza na anayehusika.

Serikali imeilekeza Idara ya Usambazaji wa Umeme ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuchukua hatua kwa yeyote atakayehusika na kuwapa kazi na mikataba Wakandarasi wa Usambazaji wa vifaa vya umeme ambao hawana uwezo wa kufanya kazi hiyo ama wanaofanya kazi kwa uzembe.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi ambayo inafanyika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme katika Kituo cha Kupoza umeme cha Ilala Jijini Dar Es Salaam.

Amesema Idara hiyo iwasimamie wakandarasi waliopewa mikataba ya kazi ya kusambaza vifaa kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye njia za kusambaza umeme ambazo zinapeleka umeme kwa wananchi ili vifaa hivyo vipatikane kwa wakati kwa kuwa upatikaji wake umekuwa unasumbua.

“Kwa hiyo kama unafanya uzembe kwa kuwapa kazi na mikataba wasambazaji ambao hawana uwezo au wanaoshindwa kufanya kazi na hamuwachukulii hatua tutaanza na anayehusika, pamoja na hao wakandarasi kwa sababu tumewaelekeza maeneo hayo ni mjini ni lazima wananchi hao wapate umeme wa uhakika”, alisisitiza Mhe. Kapinga.

Sambamba na hilo ameagiza Idara ya Usambazaji kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kama mkandarasi aliyepewa kazi hatekelezi kwa wakati majukumu yake na kufanya kazi kwa uzembe asiongezewe mkataba wake pale utakapokwisha badala yake wawapatie kazi wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza kazi zao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa vinavyohitajika kama Nguzo, Mashineumba, Waya na vifaa vingine muhimu katika maeneo husika.

Share: