Mchungaji amtapeli muumini milioni 35

Muumini wa kabisa Moja nchini Kenya amehamia kortini akitaka arudishiwe Ksh2.6 milioni (Tsh 35 milioni) kutoka kwa Mchungaji katika mpango wa biashara ambao haukukamilika.

Kulingana na mwanamke huyo, uamuzi wake wa kutuma pesa hizo kwa Mchungaji bila makubaliano ulitokana na imani yake kwake kwani alikuwa mtu wa Mungu na hakutarajia angemlaghai.

Mwanamke huyo alidai kuwa Mchungaji huyo ambaye alikutana naye miaka kadhaa iliyopita, alitakiwa kumnunulia na kumtunza ng’ombe nyumbani kwake baada ya kumhakikishia uwezo wa kufanya hivyo anao.

Hata hivyo, mwanamke huyo alithibitisha kwamba majaribio yake ya kumtembelea Mchungaji huyo yaliambulia patupu baada ya kuwa na mawasiliano magumu nae.

Pia alidai kuwa Mchungaji huyo, alimshawishi kuwa ng’ombe hao walikuwa wakienda malishoni katika mashamba mengine kila alipoonyesha nia ya kumtembelea nyumbani kwake.

Zaidi ya hayo, alieleza kwamba alituma pesa hizo kwa Mchungaji kupitia huduma za pesa za simu, huku akitoa Ksh1,020,000 milioni kutoka kwa benki yake ambayo alituma kupitia nambari zake mbili za simu.

“Nilimwamini sana mchungaji na sikupingana na lolote alilosema kiasi kwamba sikuwahi kuingia naye makubaliano,” alisema bibi huyo.

Akiongea mahakamani mwanamke huyo pia alifichua kuwa hapo awali alitoa gari alilomnunulia Mchungaji huyo kwa ajili ya upako.

Hata hivyo, alieleza kuwa baadaye, Mchungaji aliimiliki kwa muda wa miezi sita na kusema kwamba hakuwa amemaliza maombi hayo hadi DCI ilipoingilia kati kumsaidia kutwaa tena.

Share: