Mchawi adaiwa kuanguka na ungo Tanesco akiwa katika safari zake Ruvuma

Hali ya taharuki inadaiwa kutanda katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, baada ya mwanamke mmoja, ambaye jina lake halijafahamika, kukutwa akiwa uchi ndani ya ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambapo inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa akisafiri kutoka Masasi Mkoani Mtwara kuelekea Nyasa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa usiku kuamkia Machi 11, 2025.

Kamanda Chilya ameeleza kuwa baada ya mwanamke huyo kukutwa katika eneo la jengo la TANESCO na umati wa watu kuanza kukusanyika, uongozi wa shirika hilo ulitoa taarifa kwa Kituo Kikuu cha Polisi Songea.

Askari polisi walifika haraka eneo la tukio na kumkuta mwanamke huyo akiwa uchi wa mnyama, huku akiwa amejificha kwenye moja ya vyoo vya ofisi hizo. Baada ya mahojiano ya awali, maafisa wa polisi waliamua kumpeleka Hospitali ya Mkoa wa Songea (HOMSO) kwa uchunguzi zaidi ili kubaini hali yake ya kiafya, hasa ikiwa anatatizo la afya ya akili.

Kwa sasa, amelazwa katika wodi namba nane akisubiri uchunguzi wa kitaalamu.

Athumani Mohamed, mkazi wa Mtaa wa Ruvuma, amesema inadaiwa kuwa mwanamke huyo alipita karibu na Kanisa la Pentekoste REDMD (Walokole) ambapo alipoteza mwelekeo, na hatimaye akaanguka ndani ya uzio wa ofisi za TANESCO akiwa uchi huku usoni akiwa amejipaka unga mweupe.

Share: