Makonda apigilia msumari challenge ya wanaume kuwapost wake zao

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesisitiza umuhimu wa "challenge" yake aliyoianzisha Jana Jumapili, ikianza utekelezaji wake leo Jumatatu Machi 03, 2025, akiwaambia wanaume kuwa kuchapisha (Kupost) picha ya Mkeo ama mpenzi wako mtandaoni kwenye Juma hili la siku ya mwanamke kunaongeza kujiamini na kujisikia fahari kwa mwanamke uliyenaye kwenye mahusiano.

Leo jumatatu wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokutana na Vilabu vya kandanda vya wanawake vinavyoshiriki ligi ya Samia Women Super Cup Jijini Arusha, Mhe. Makonda amewasihi wanaume wa Mkoa wa Arusha kuwapa wanawake haki hiyo kama sehemu ya kuonesha kuthamini mchango wao kupitia shughuli na majukumu yao ya kila siku ndani na nje ya familia wanazoishi.

Mhe. Makonda amesisitiza kuwa kwa wanawake ambao wanaume wao hawatoshiriki kwenye "challenge" hii itakayokoma Ijumaa ya wiki hii, siku ya Jumamosi atatoa tathmini na mbinu za kujikwamua kwa wanawake hao kwenye mahusiano hayo ambayo wamekuwa nayo na wanaume wao wameshindwa kuonesha kuwathamini na kushiriki kwenye zoezi hilo lililoanza mapema leo Jumatatu, akitahadharisha wanaume kwamba kuwa na wanawake wengi ni gharama na hakuna faida yeyote ya kuwa na msururu wa wanawake.

Share: