Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ili kuufanya Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma kuwa endelevu, ni muhimu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Halmashauri husika kuhakikisha upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa nyumba za watumishi yaliyo karibu zaidi na sehemu za kazi na yanayozingatia mahitaji ya msingi ya watumishi na familia zao kwa sasa na kwa wakati ujao.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma unaotekelezwa na Taasisi ya Watumishi Housing Investments katika hafla iliyofanyika katika eneo la Njedengwa Mkoani Dodoma. Amesisitiza nyumba zinazojengwa lazima zizingatie ubora na viwango stahiki ili kuendana na thamani ya fedha na kuwaepusha wanunuzi wa nyumba hizo gharama za marekebisho na maboresho zaidi.
Makamu wa Rais amesema ili mpango huo uweze kufikia malengo yake na kuwa na manufaa kwa watumishi, ni muhimu vigezo na masharti ya upatikanaji wa nyumba kwa watumishi wa umma viheshimiwe na kuzingatiwa. Amesisitiza upokeaji, uchambuzi wa maombi na uthamini wa nyumba hizo vifanyike kwa haki na kuzingatia uhalisia. Amesema juhudi za makusudi zifanyike ili watumishi wa ngazi za chini na kati wapewe kipaumbele katika upatikanaji wa nyumba hizo.
Ametoa wito wa kuzingatia uwepo wa viwanja vya michezo, maeneo ya kupumzikia na huduma nyingine za jamii kama elimu, afya na huduma za mahitaji ya maisha, kama maduka na maeneo ya ukusanyaji wa taka wakati wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa watumishi na wananchi ambao watapata nafasi ya kununua nyumba hizo kuzitunza ili zibaki katika hali ya ubora kadri inavyowezekana ikiwemo miundombinu na mazingira yanayozunguka eneo la nyumba. Amewahimiza kupanda miti na maua ili kuleta mandhari nzuri na pia kuhakikisha usafi muda wote.
Makamu wa Rais amesema Serikali imedhamiria kuona miradi hiyo inatekelezwa katika mikoa na wilaya zote nchini ili kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya Watumishi wa Umma wanaishi katika nyumba bora, na hivyo kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Amesema pamoja na kupunguza uhaba wa makazi, pia mradi huo ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kutoa ajira na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya ujenzi, hususan wa makazi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesema thamani ya uwekezaji uliyofanywa katika mfuko wa uwezeshaji katika miliki ambazo zinatoa fedha kuwezesha mpango huo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 57.9 mwaka 2013/2014 hadi kufikia bilioni 69.7 Juni 2024. Amesema ukuaji huo umetoa gawio la shilingi bilioni 1.8 kwa wawekezaji wake na hadi kufikia mwaka wa fedha 2022/2023 Watumishi Housing Investments imekamilisha miradi yenye thamani ya bilioni 87.97.
Awali akitoa taarifa za mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Watumishi Housing Investments Dkt. Fred Msemwa amesema Taasisi hiyo imekuwa ikichukua hatua za kutafuta fedha za ujenzi wa nyumba na kuhakikisha nyumba hizo zinauzwa kwa bei nafuu pamoja na watumishi wa umma kuwekewa mifumo ya kukuza fedha zao ili wawe na uwezo wa kununua nyumba na kufanya majukumu mengine ya kiuchumi yanayozikabili familia zao.
Jumla ya nyumba za makazi 1006 katika mikoa 19 zimejengwa na Taasisi ya Watumishi Housing Investments kwa lengo la kuwawezesha watumishi kupata nyumba bora za kuishi kwa gharama nafuu. Katika hafla hiyo Nyumba 206 zimezinduliwa zilizojengwa katika eneo la Njedengwa mkoani Dodoma.