Maandamano ya agadez kaskazini mwa niger yatoa wito wa kuondoka mara moja kwa wanajeshi 1,000 wa marekani walioko huko

Mamia ya watu wamefanya maandamano huko Agadez kaskazini mwa Niger, wakitoa wito wa kuondoka mara moja kwa wanajeshi 1,000 wa Marekani walioko huko.

Maandamano hayo ya Jumapili yaliitishwa na mashirika yanayounga mkono mamlaka ya kijeshi ambayo yalichukua uongozi mwaka jana.

Tukio hilo limefanyika siku mbili baada ya Marekani kukubali kuondoa vikosi vyake katika taifa la Sahel kujibu uamuzi wa mwezi uliopita wa serikali inayoongozwa na jeshi mjini Niamey ya kubatilisha makubaliano yaliyoruhusu majeshi ya Marekani kufanya kazi nchini humo.

Marekani pia ilikubali kufunga kambi ya ndege zisizo na rubani kutoka eneo ambapo inendesha operesheni dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Kiislamu.



"Ujumbe wetu uko wazi: Wanajeshi wa Marekani, bebeni virago vyenu na muende nyumbani," mmoja wa waandamanaji aliambia shirika la habari la AFP.

Waandamanaji walionekana wakiwa wamebeba bendera za Urusi, pamoja na Burkina Faso, Mali na Niger.

Viongozi wa kijeshi katika nchi hizi wamekuwa wakiimarisha uhusiano na Moscow.

Niger iko katika eneo la Sahel barani Afrika, ambalo linachukuliwa kuwa kitovu kipya cha kimataifa cha kundi la Islamic State.

Marekani imeitegemea Niger kama kambi yake muhimu kwa kufuatilia shughuli za kikanda za wanajihadi.



Makumi ya wakufunzi wa kijeshi wa Urusi wamewasili Niger katika wiki za hivi karibuni, wakileta mfumo wa hali ya juu wa ulinzi wa anga, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya serikali.











Share: