Kenya yataka kuondoa raia wake kwenye machafuko DRC

Serikali ya Kenya imependekezea raia wake kuondoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutokana na kuongezeka kwa ghasia kati ya vikosi vya usalama na waasi wa M23.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama na aliziagiza familia za Wakenya kuchukua tahadhari, huku akisisitiza wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa pamoja wa viongozi wa kanda uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania, kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

“Kenya ina wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mizozo huko DRC,” alisema waziri huyo.

Akirejea mashambulizi dhidi ya ofisi za ubalozi wa Kenya mjini Kinshasa waziri huyo pia alisisitiza juhudi za kidiplomasia kutafuta amani.

Aidha, wakazi wa mji unaopakana na Burundi , unaojulikana kama Uviru wameingiwa na hofu haswa waliozungumza na BBC wakisema M23 tayari wamesogelea eneo hilo.

Haya yanajiri siku chache baada ya waasi wa M23 kudhibiti Bukavu na Goma, miji ambayo ina wakazi wengi DRC. Kwa upande mwingine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeomba msaada wa kijeshi kutoka Chad katika jitihada zake za kupambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika mikoa yake ya mashariki.

Share: