"Mitandao ya kijamii na majukwaa ya SMS ni uwanja mpya wa umma. Nafasi za umma kwa mijadala ya umma. Jamii ya Kenya inasalia kugawanyika kuhusu kile kinachochochea unyanyasaji wa kingono na kijinsia.
Mauaji ya kikatili ya msichana Mkenya katika nyumba ya kupangisha kwa muda mfupi yamezua ghadhabu na kufichua "taasubi kali' ya kiume inayoendeleza chuki dhidi ya wanawake mtandaoni nchini.
Mwanamke huyo alikatwa vipande na mabaki yake yakatupwa kwenye mfuko wa plastiki, kulingana na ripoti ya polisi ambayo BBC iliiyona. Polisi wanachunguza lakini mshukiwa bado yuko huru.
Kesi hiyo imemwacha mkurugenzi mkuu mtendaji wa Amnesty International Kenya Irungu Houghton akiwa "ameshtuka na kughadhabishwa".
"Mwanamke mwingine katika miaka yake ya 20 ambao hawataweza kutimiza miaka yake ya 40," alisema.
Chini ya wiki mbili zilizopita, sosholaiti Mkenya pia aliuawa katika nyumba ya kukodisha kwa muda mfupi katika mji mkuu, Nairobi.
Unyanyasaji wa kijinsia ni tatizo kubwa nchini Kenya. Mnamo 2022 takriban 34% ya wanawake walisema walipitia ukatili wa kimwili, kulingana na utafiti wa kitaifa.
Mauaji haya ya hivi punde yametoa mwanga kwenye kona ya giza ya mitandao ya kijamii ya Kenya ambayo imeelezwa kuwa "manosphere", ambapo maoni mengi yameshirikishwa yakiwalaumu wanawake kwa vifo vyao wenyewe.
"Manosphere" ni mtandao wa majukwaa ya mtandaoni ambayo yanalenga katika kukuza 'uanaume' au taasubi zake na kufanya kazi kinyume na ufeministi.
Mwanaume mmoja Mkenya kwenye X, ambaye zamani ilijulikana kama Twitter, alisema: "Kwa kweli nadhani hakuna unaharakati wowote utakaokomesha mauaji ya wanawake."
Aliongeza kuwa ni juu ya "wanawake kutanguliza usalama wao", akidai ndilo "chaguo linalowezekana".
Ili kujibu mtindo huo wa kuwalaumu waathiriwa kauli mbiu ya , "ACHENI KUUA WANAWAKE" ilianza kuvuma nchini Kenya kwenye X.
Mwanamke mmoja kwenye X alisema: "Hatuwezi kuamini bado tunaona hadithi za kile ambacho wanawake wanapaswa na hawapaswi kufanya wakati wanaume wanapaswa kuacha kuua wanawake kwanza," akiongeza kuwa "Ni rahisi sana."
Mbunge wa Kenya Esther Passaris aliiambia BBC kuwa hakushangazwa na muathiriwa anayelaumiwa mtandaoni kwa sababu Kenya ni jamii ya mfumo dume, na inawadharau wanawake.
Anasema kuwa kama mwanamke , amekuwa akilengwa na maneno ya dharau na mara nyingi huitwa "kahaba".
Kwa wanakampeni wengi, kauli kutoka kwa wanaume wa Kenya mtandaoni si jambo geni.
Bw Houghton aliiambia BBC kuwa maoni haya hayakuwa tu matukio ya pekee ya wanaume wasiopenda wanawake lakini yalikuwa ni dalili ya utamaduni mpana wa "kuchukia wanawake".
"Mitandao ya kijamii na majukwaa ya SMS ni uwanja mpya wa umma. Nafasi za umma kwa mijadala ya umma. Jamii ya Kenya inasalia kugawanyika kuhusu kile kinachochochea unyanyasaji wa kingono na kijinsia.
"Kwa baadhi, kulaumu wanawake na kwa wengine kulaani wanaume ni hoja zinazokubalika," Bw Houghton alisema.
Onyango Otieno, mwanaharakati mwenye umri wa miaka 35, ambaye anapinga masimulizi mabaya ya kuendeleza mfumo dume , aliambia BBC kwamba wanaume hutamka lugha ya dharau kwa sababu "ahadi ya mfumo dume" inaondolewa huku wanawake wakitaka usawa zaidi.
Anasema wanaume wa Kenya wameshawishika na jamii kuamini kuwa nafasi yao ni juu ya wanawake, lakini kuongezeka kwa ufeministi kumewaacha wanaume wengi wakihisi wamedhoofika au nafasi yao kuchukuliwa na wanawake.
“Wanaume wengi hawakufundishwa wala kuelimishwa jinsi ya kuishi pamoja na wanawake wakiwa binadamu sawa,” Bw Otieno anapumua.
Anasema wanaume wengi wanapambana na ukweli huu. "Manosphere" kwa maana fulani ni njia ya kupigania "ahadi ya mfumo dume".
"Dunia imebadilika kwa njia nyingi sana. Wanaume hawajabadilika," anasema kwa uhakika.