Kamati ya tamisemi yatoa ushauri manispaa ya tabora

Mhe. Nyamoga ameshauri viongozi wa Manispaa ya Tabora kurekebisha kasoro zilizonekana katika shule ya msingi ya Miyemba

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa ushauri na kuwataka watendaji waliopewa dhamana kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya ujenzi wa miradi katika maeneo yao kwa kufika site na sio kukaa ofisini.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Justine Nyamoga amesema, kama viongozi watafuatilia miradi ni rahisi kujua changamoto, kasoro za miradi inayotekelezwa mapema na kuzifanyia kazi mapema kabla ya mradi huo haujakamilika chini ya kiwango na kuwa na hasara kubwa baadae.

Amesema fedha nyingi Serikali inatoa kujenga miundombinu ya elimu kama miradi hiyo haitasimamiwa vizuri itakua ni hasara kwa Taifa na maana yake viongozi waliopewa dhamana watakua wameshindwa kumsaidia Mhe.Rais ambaye nia yake nikusaidia wananchi.

Mhe. Nyamoga ameshauri viongozi wa Manispaa ya Tabora kurekebisha kasoro zilizonekana katika shule ya msingi ya Miyemba wakati wa ziara ya Kamati hiyo.

Pia wametoa wito kwa viongozi wote wa Halmashauri kufuata maelekezo na miongozo ya michoro ya ujenzi wa miradi hiyo ya shule wanayopewa bila ya kusahau kujenga vyumba vya kujihifadhia kwa wanafunzi wa kike.

Kwa upande wa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Deogratius Ndejembi ameishukuru Kamati na kusema yote waliyoyaelekeza yatashughulikiwa kwa kufanyiwa kazi mapema.

Share: