John Mnyika maoni ya Chadema juu ya kushughulikia miswada ya uchaguzi nchini Tanzania yamepuuzwa.

Katibu wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema, John Mnyika amesema kuwa maoni yao na ya wadau juu ya kushughulikia miswada ya uchaguzi nchini Tanzania yamepuuzwa.

Moja ya agenda ya maandamano yaliyofanywa na chama hiko siku chache zilizopita ni kushinikiza miswada hiyo kuondolewa bungeni.

Kupitia ujumbe alioweka katika mtandao wa X, Mnyika ameelezea ratiba iliyowekwa kwenye tovuti ya Bunge, akisema kuwa ‘’miswada mibovu ya uchaguzi na vyama itajadiliwa kuanzia leo mpaka tarehe 2 Februari 2024’’.

‘’Inakwenda kupitishwa bila kuanza na mabadiliko au marekebisho ya katiba’’ Mnyika alisema.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wiki iliyopita alisema maandamano hayo yalilenga kuishinikiza serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi.

Vilevile chama hicho kiliitaka serikali iondoe Bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi, ambayo ni muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa na Sheria ya gharama za Uchaguzi.

Badala yake, Chadema iliitaka serikali iwasilishe muswada wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia mwafaka wa kitaifa.

Kadhalika, Chadema iliitaka serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na ule mkuu wa 2025 uwe huru na haki.

Katika taarifa ya Bunge la Tanzania, mkutano huo umeongezewa wiki moja ya ziada ili kujadili kwa uzito miswada hiyo.

‘’Mkutano huu umeongezewa wiki moja kutokana na uzito wa majukumu yaliyopangwa ikiwemo uzito wa Miswada itakayoshughulikiwa”

Share: