Jeshi la polisi linachunguza Tukio la utekaji wa Deogratius Tarimo

Jeshi la Polisi nchini linachunguza picha mjongeo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha watu ambao wanajaribu kumkamata na kujaribu kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari Mfanyabiashara na Mkazi wa Kibaha mkoa wa Pwani Deogratius Tarimo.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime imeeleza kuwa tukio hilo liliripotiwa na mfanyabiashara huyo (Deogratius Tarimo) katika Kituo cha Polisi Gogoni, Dar es Salaam Novemba 11, 2024.

"Kulingana na ushahidi uliowasilishwa kituoni hapo na yeye mwenyewe ni kwamba, chanzo cha tukio na kilichomsukuma kufika katika Hoteli ya Rovenpic iliyopo eneo la Kiluvya Jijini Dar es Salaam ni kufanya mazungumzo ya biashara ambayo amekuwa akiwasiliana kuifanya na aliokuwa anawasiliana nao toka Oktoba 25, 2024".



Jeshi la Polisi linahakikisha litawakamata watu waliokuwa wakijaribu kumkamata na kujaribu kumwingiza kwenye gari mfanyabiashara huyo kama inavyoonekana katika picha mjongeo hiyo kulingana na ushahidi ambao umekwishakusanywa na unaoendelea kukusanywa ili hatua zingine ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria kwani hakuna aliyejuu ya Sheria" imesema taarifa hiyo ya David Misime.


Share: