Israel yashambulia makazi ya kiongozi wa hamas

Kulingana na jeshi la Israel, makazi hayo ya Haniye mara kwa mara yalitumika kama eneo la mikutano ya viongozi wa juu wa Hamas. Jeshi hilo limesema makazi hayo yalikuwa yakitumika kama sehemu ya miundombinu ya kigaidi na mara kwa mara yalitumika kama eneo la mikutano ya viongozi wa juu wa Hamas.

Jeshi la Israel limebainisha kwamba ndege zake za kivita zimeyashambulia makaazi ya Ismail Haniye anayeongoza Ofisi ya masuala ya kisiasa ya kundi la Hamas. Taarifa za mashambulizi hayo zimetolewa katika chapisho lililoambatana na video ya mashambulizi hayo katika ukurasa wa jeshi la Israel la mtandao wa kijamii wa X uliokuwa ukijulikana awali kama twitter. 

Hata hivyo duru za habari zinasema, Haniyeh,ambaye makazi yake yamelengwa na mashambulizi ya Israel amekuwa akiishi nchini Qatar tangu mwaka 2019 pamoja na familia yake. Kulingana na ripoti kutoka vyanzo ndani ya Hamas, hakukuwa na mtu ndani ya nyumba hiyo wakati wa mashambulizi.

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Israel Isaac Herzog amezungumzia mustakabali wa hali ya usalama ya Ukanda wa Gaza inavyoweza kuwa hapo baadaye. Herzog amesema Israel haiwezi kuondoka kirahisi Gaza kwani eneo hilo haliwezi kuachwa namna lilivyo sasa. Amefafanaua zaidi na kuongeza kuwa ili kuzuia ugaidi kujitokeza tena, wanapaswa kuwa na kikosi madhubuti kuhakikisha kuwa shambulio kama la Oktoba 7 halijitokezi tena.

Share: