Imamu apigwa risasi na kuuawa nje ya msikiti marekani

Imamu wa msikiti mmoja huko Newark, New Jersey, amepigwa risasi na kuuawa mapema Jumatano asubuhi na mshambuliaji asiyejulikana ambaye bado anasakwa.

Imam Sharif alipatikana na majeraha mengi ya risasi nje ya msikiti wake, Masjid-Muhammad-Newark, kabla ya mapambazuko. Alipelekwa hospitali na baadaye alifariki dunia kutokana na majeraha.

Gavana Phil Murphy alitoa taarifa akiomba yeyote aliye na habari kuhusu mshambuliaji ajitokeza na zawadi ya dola za kimarekani 25,000 itatolewa kwa yeyote atakayejitokeza na habari za mshambuliaji.

Seneta wa New Jersey, Cory Booker ameandika kupitia X, "amehuzunishwa na kifo cha kupigwa risasi cha Bw Sharif na kusema moyo wake uko pamoja na waumini wa Masjid Muhammad na Waislamu wote wa New Jersey.''

Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu la New Jersey lilisema "limehuzunishwa na habari za kuuawa kwa Imamu Sharif na kumtaja kama kinara wa uongozi bora."

Sharif alifanya kazi kama afisa wa usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Newark Liberty kwa miaka mingi huku akiwa na majukumu yake msikitini.

Share: