Dkt. biteko ataka sekta ya uvuvi iwe nyenzo ya kuondoa umaskini nchini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaagiza watendaji wa Sekta ya Uvuvi nchini kuifanya Sekta hiyo kuwa nyenzo muhimu ya kuondoa umaskini nchini.


Amesema, lengo ni kuiwezesha Sekta ya Uvuvi iwe na mchango mkubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Biteko ameyasema hayo  wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) sambamba na kuzindua mfumo maalum wa upatikanaji wa taarifa sahihi za uvuvi na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya TAFIRI na ZAFIRI kwenye mazao ya bahari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Hakikisheni kuwa, Wizara pamoja na TAFIRI mnakuwa kimbilio la wavuvi wakiwaona ninyi wajue majibu ya maswali yao watayapata kwenu, na muone fahari ya kuwaona wavuvi wanakuwa matajiri,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ameitaka TAFIRI kuongeza mchango wa mauzo ya bidhaa nje ya nchi ili kuweza kuleta fedha zaidi za kigeni ambayo imekuwa changamoto kubwa kwenye uchumi wa nchi. Amesema kuwa, “Mauzo ya bidhaa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 168 mwaka uliopita hadi kufikia Dola za Marekani milioni 249,” ameeleza Dkt. Biteko.

Share: