Dk. Biteko atoa maagizo kuhusu sera ya michezo mahali pa kazi

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dk Doto Biteko, ameiagiza Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni, kukamilisha Sera ya Michezo Mahali Pa kazi, ili kuwabana waajiri wasiotambua umuhimu wa sekta hiyo kwa watumishi.

Mhe Dk Biteko, ametoa agizo hilo wakati akifungua michezo ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA) Novemba 18, 2024 kwenye uwanja wa Usagara jijini Tanga.

Amesema, kuna waajiri na menejimenti ambazo, licha ya Serikali kuweka utaratibu wa michezo inayohusisha asasi za umma na binafsi, wanashindwa kuwawezesha watumishi wao kushiriki, huku wakitumia sababu zisizokuwa na uzito ikiwemo ufinyu wa bajeti.

 

Mhe Dk Biteko amesema, wakati ufinyu wa bajeti ukitumika kama kikwazo, viongozi wa asasi husika wamekuwa wakishiriki ziara zikiwemo za mafunzo na semina nje ya maeneo yao ya kazi, kwa kugharamiwa na taasisi zao.

Amesema, kwa vile ilishakubalika Serikalini kuhusu kufanyika kwa mashindano ya michezo kupitia mashirikisho mbalimbali, ipo haja kwa Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni ‘kuja’ na sera hiyo itakayotumika kuhimiza watumishi kushiriki kwenye michezo.

Mhe Dk Biteko ametoa mfano kuwa, ongezeko la taasisi washiriki wa SHIMMUTA kutoka 57 wa mwaka jana kufikia 97 mwaka huu, ni ishara nzuri ya utekelezaji wa maagizo yake, ingawa idadi hiyo inapaswa kuongezeka kufikia mashirika ya umma, taasisi na makampuni binafsi yanayofikia 304.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mh Balozi Dk Burian, amesema mkoa huo unaendeleza michezo, sanaa na burudani kama inavyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi na kutoa mfano, wakazi wake wameshiriki kwa mafanikio makubwa kwenye Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililofanyikia Havana, Cuba Novemba 7-10, mwaka huu.

Share: