Dcea: polisi inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha magunia 205 ya madawa ya kulevya

Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha magunia 205 yanayodhaniwa kuwa na dawa ya kulevya aina ya bangi.

Watu hao walikuwa wakisafiri na magunia hayo kutoka wilayani Tarime kuelekea Dar es Salaam kwa kutumia gari aina ya Iveco na kuficha magunia hayo katika tenki la kubebea mafuta.

Watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa wamekamatwa alfajiri ya leo na wanashikiliwa katika kitua cha Polisi mjini Bunda.

Akizungumzia tukio hilo, Wakili Mkuu wa Serikali, Christina Rweshabura ambae amemwakilisha Kamishna Jenarali Mkuu wa DCEA amesema taasisi hiyo imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha inakomesha biashara hiyo haramu nchini.

Amesema DCEA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wataendelea na uchunguzi na kisha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vicent Naano amewaonya wote wanaojihusisha na vitendo vya usafirishaji sambamba na matumizi ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani mkono wa Serikali ni mrefu na katu mkoa huo hauko tayari kutumika kama njia ya usafirishaji wa dawa za kulevya.

Share: