Dawasa kuendelea kutatua changamoto za kutopatikana kwa huduma ya maji

Kuna baadhi ya maeneo ambayo bado tunaendelea kuimarisha, tunaelekea eneo ambalo pia bado lina changamoto

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imesema inaendelea kutatua changamoto ya kutopatikana kwa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo changamoto ambayo inatokana na msukumo mdogo wa maji “low pressure”.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro ameyasema hayo wakati wakitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo Luguruni, Magari saba, Ubungo, Ilala na Kinondoni kujionea hali ya upatikanaji wa maji.

“Kwa muda mfupi kidogo tulipata changamoto ya msukumo mdogo wa maji ambapo maeneo mengi maji yamekuwa yakipatikana kwa kiasi kidogo na kwa siku chache lakini baada ya timu ya Wataalamu kukaa na kuangalia namna nzuri ya kufanya kuwezesha kurejesha huduma kama awali, tumefanya maboresho makubwa yaliyohusisha kuongeza msukumo wa maji katika mabomba makubwa yanayotoka Ruvu Juu na Ruvu chini, hali ya maji inazidi kuimarika”

“Kuna baadhi ya maeneo ambayo bado tunaendelea kuimarisha, tunaelekea eneo ambalo pia bado lina changamoto mfano Kinyerezi, Kisukuru, Kanga, Mongolandege yote yapo Wilaya ya Ilala wanapata maji kidogo, nako tunaendelea na maboresho yetu”

Alipoulizwa kuhusu mgao wa umeme kuathiri usambazaji wa maji, Everlasting amesema yafuatayo “Serikali imetamka kwamba inaelekea ukingoni kumaliza mgao wa umeme na hakuna maji bila umeme na hakuna umeme bila maji, tunategemeana kwahiyo changamoto ya umeme itapoisha basi na huduma zetu zitaendelea kuimarika”





Share: