Dar yatoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wahanga wa mafuriko hanang-manyara

DSM ni mji muhimu kwa mengi ikiwemo biashara, diplomasia, na uchumi hivyo tatizo lolote likitokea litagharimu maisha ya wengi, "Natoa wito kwa wakazi wa DSM kuilinda DSM kama mboni ya jicho kwa maslahi mapana ya taifa letu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila, leo Desemba 6, 2023 ametoa Salamu za pole na msaada wa vifaa mbalimbali kwa waathirika wa maafa ya mafuriko Wilaya ya Hanang Mkoa wa Manyara.

Akiongea na Waandishi wa Habari wakati wa kutoa vifaa hivyo RC Chalamila amesema viongozi wote wa wilaya za Mkoa wa DSM na wadau wanaungana na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa pole na kuwasitiri wahanga wote wa mafuriko kwa kutoa vifaa mbalimbali vikiwemo magodoro 250, mablanketi ya wakubwa 1200 na ya watoto 300, sabuni  katoni 100, mikeka 500, ndoo ndogo ( Lt 10) 350 na kubwa (Lt 20) 350, sahani 500 na seti za kupikia 20.

"Tunatoa pole kwa watanzania wenzetu ambao wamefikwa na maafa hayo, sisi wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mimi Mkuu wa mkoa tunaungana pia na viongozi wa Mkoa wa Manyara na hasa hasa kumpa pole za dhati kabisa Mhe Queen Sendiga ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara," alisema RC Chalamila

Vilevile RC Chalamila amesema majanga yaliyotokea Hanang yachukuliwe kama somo na yanaweza kutokea sehemu yoyote, hivyo alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam kuendelee kuchukua tahadhari, kuhama  mabondeni, kufungua njia za maji, kufanya usafi ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Pia Mhe Chalamila amesema mkoa wa DSM ni mji muhimu kwa mengi ikiwemo biashara, diplomasia, na uchumi hivyo tatizo lolote likitokea litagharimu maisha ya wengi, "Natoa wito kwa wakazi wa DSM kuilinda DSM kama mboni ya jicho kwa maslahi mapana ya taifa letu," alisisitiza.

Mwisho ikumbukwe kuwa Desemba 3 mwaka huu wakazi wa Hanang walikumbwa na mafuriko ya maji yaliyoambatana matope, mawe na magogo na kusababisha vifo na majeruhi kwa watu na mifugo, na uharibifu wa miundombinu.

Share: