Bashungwa aagiza kazi kuondoa tope katika mji wa katesh ifanyike usiku na mchana.

Waziri wa Ujenzi, Innocent. Bashungwa amewaagiza wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini ( TARURA) kwa pamoja kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ya kuondoa tope kwenye makazi ya watu na kwenye miundombinu katika mji wa katesh Wilayani Hanang.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo wakati alipoambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista J. Mhagama, Waziri wa Madini, Anton Mavunde kukagua hali ya miundombinu na kujionea jitiada za uokoazi unaoendelea, leo tarehe 4 Disemba 2023.

“TANROADS shirikianeni kwa pamoja na TARURA kwa kuongeza mitambo na vifaa ili kazi ya kuondoa tope ifanyike usiku na mchana katika maeneo yote ya mji wa Katesh ikiwa ni pamoja na humu kwenye makazi ya watu, Sokoni na kwenye miundombinu ya barabara,” amesema Bashungwa

Waziri Bashungwa amesema Serikali itahakikisha inafanya kila jitihada ambazo zitaruhusu shughuli za uzalishaji zinaendelea kama kawaida na maisha yarejee kama ilivyokuwa awali. 

Amemtaka Meneja wa TANROADS mkoa Manyara kuhakikisha mitambo na vifaa vyote vinakuwa na mafuta na kazi ifanyike usiku na mchana bila kuwepo na kikwazo wala sababu yoyote.

Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista J. Mhagama amesema kazi ya uokozi inaendelea ikiwa ni pamoja na utafutaji wa miili inayosadikika bado haijapatikana.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanagharamia shughulia za mazishi, ikiwa na kutoa matibabu bure na huduma zote kwa waathirika wa maafa haya.

Waziri Jenista amesema wanajipanga kuhakikisha wanarejesha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na umeme, maji na huduma nyingine za kijamii zilizoathiriwa na maafa hayo.

Share: