Barabara ya kibada mwasonga-kimbiji km 41, kujengwa kwa kiwango cha lami

Eng. Dorothy Mtenga amesema Barabara hiyo ni moja ya Barabara za muhimu kwa mkoa wa Dar-es Salaam kwani inapita sehemu zenye uwekezaji na idadi kubwa ya watu

Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kibada_Mwasonga_Kimbiji yenye urefu wa km 41 wilayani Kigamboni.

Waziri wa Ujenzi Mh.Innocent Bashungwa amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali za kuiwezesha wilaya ya Kigamboni kuwa na barabara nyingi za lami na hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wake.

"Mh.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amenituma nije nikague barabara hii ambayo ujenzi wake utaanza hivi karibuni", amesema Mh. Bashungwa.

Aidha, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es salaam Eng. John Mkumbo kuendelea kuikarabati barabara hiyo ili ilipitike wakati wote wakati maandalizi ya kuijenga kwa lami yakiendelea. 

Kufuatia ombi la Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo la kuiomba Serikali kujenga kipande cha Km 7, kutoka Kimbiji hadi Cheka ambacho ni muendelezo wa barabara hiyo Waziri Bashungwa amamuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam kufanya usanifu katika sehemu hiyo wakati yeye akifuatilia kibali cha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ili kuiwezesha barabara yote kujengwa kwa lami.

Kaimu Mtendaji mkuu wa TANROADS Eng. Dorothy Mtenga amesema Barabara hiyo ni moja ya Barabara za muhimu kwa mkoa wa Dar-es Salaam kwani inapita sehemu zenye uwekezaji na idadi kubwa ya watu.

"Barabara hii ikikamilika itachochea uchumi wa wananchi wa Kigamboni na kutengeneza mtandao mzuri wa barabara za lami ", amesisitiza Eng. Mtenga.

Waziri Bashungwa amehitimisha ziara yake ya siku tatu jijini Dar-es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine ametembelea Wilaya zote 5 za mkoa huo ambazo ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni na kukagua athari za mvua za vuli na kutoa maelekezo kwa TANROADS, Wakandarasi na wananchi hususan kutovamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kuzilinda barabara ili zidumu kwa muda mrefu.

Share: