Mkoa wa Arusha utakuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa 73 wa Baraza la Kimataifa la viwanja vya ndege kwa Kanda ya Afrika utakaowakutanisha Wataalamu mbalimbali kutoka kwenye mashirika ya ndege, Makampuni na taasisi za Kimataifa za usafiri wa anga zaidi ya 400, ukitarajiwa kufanyika kwa siku saba kuanzia Aprili 24- 30, 2025.
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Kwenye ukumbi wa Mikutano uwanja wa ndege Arusha wakati akizungumza na wanahabari leo Januari 08, 2025, amesema maandalizi ya mkutano huo yanakwenda vizuri, akiushukuru Uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mhe. Paul Christian Makonda kwa ushirikiano wao, akiwasihi wakazi wa Arusha kutumia ujio wa wajumbe wa mkutano huo kujipatia kipato na kujinufaisha Kiuchumi.
Kwa upande wake Mhe. Paul Christian Makonda aliyeambatana na Mhe. Mbarawa, ameshukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wizara hiyo kwa Kuiteua Arusha kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, akiahidi usalama wa kutosha pamoja na huduma nzuri kwenye maeneo ya malazi na kumbi za mikutano kwa wageni wote kwa siku zote saba za kufanyika Mkutano huo.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Waziri Mbarawa, Wajumbe hao zaidi ya mia nne, kwenye siku zao saba za kuwa Mkoani Arusha wametenga siku moja kwaajili ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya Utalii Mkoani Arusha suala ambalo linatajwa na Mhe. Makonda kwamba litakuwa sehemu nyingine ya kusisimua uchumi wa Mkoa wa Arusha kupitia sekta ya Utalii na sekta nyingine mtambuka za vyakula, usafiri, sehemu za starehe, hoteli na nyumba za kulala wageni.