Arusha kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania kwa maombi maalumu

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametangaza kuwa Disemba 09, 2024 wakati Tanzania itakapokuwa inaadhimisha Miaka 63 ya Uhuru, Mkoani Arusha kutafanyika Kongamano kubwa la maombi la kuombea Mkoa wa Arusha dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii ya Mkoa huo wa Kaskazini mwa Tanzania.

Mhe. Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo alipokutana na kuzungumza na Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Arusha, akisema katika maadhimisho hayo kutafanyika pia matembezi maalum kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha yakijumuisha Viongozi hao wa dini na wananchi wa mkoa wa Arusha.

"Tutatembea kwa pamoja maeneo mbalimbali mkoani Arusha tukiwa na bendera, tukitamka maneno ya baraka na maombezi kwa Mkoa wetu wa Arusha tukiombea amani, baraka, biashara zetu pamoja na kizazi tukitakacho mkoani Arusha." Amesema Mhe. Makonda.

Kauli ya Mhe. Makonda inakuja wakati huu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ametangaza kufuta sherehe za Kitaifa za maadhimisho ya Uhuru kwa mwaka 2024 na kuelekeza yafanyike katika ngazi ya mikoa huku pia akitaka fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwaajili ya sherehe hizo zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali.

Share: