Acp justine masejo: watuhumiwa 250 walikamatwa wakiwa na bangi tani sita na kilogramu 462.8

Akitoa taarifa hiyo Januari 15, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo amesema kwa Mwaka 2022 makosa ya uhalifu yalikuwa 2,995 ambayo ni tofauti na Mwaka 2023 ambapo yalikuwa 2,634 sawa na upungufu wa makosa 361.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema kwa mwaka 2023 jumla ya watuhumiwa 533 walihukumiwa Kwenda jela kwa makosa mbalimbali ikiwemo ubakaji na ulawiti huku matukio ya uhalifu yakitajwa kupungua kwa Asilimia 12.

Akitoa taarifa hiyo Januari 15, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo amesema kwa Mwaka 2022 makosa ya uhalifu yalikuwa 2,995 ambayo ni tofauti na Mwaka 2023 ambapo yalikuwa 2,634 sawa na upungufu wa makosa 361.

Kamanda Masejo amebainisha jumla ya Watuhumiwa 138 wa makosa ya Ubakaji walihukumiwa vifungo mbalimbali gerezani ambapo watuhumiwa 86 walihukumiwa vifungo vya Maisha Jela, watuhumiwa 37 walihukumiwa miaka 30 jela na wengine 15 walihukumiwa miaka 20 jela.

Aidha, kwa upande wa makosa ya ulawiti jumla ya Watuhumiwa 103 walihukumiwa vifungo mbalimbali jela ambapo watuhumiwa 89 walihukumiwa kifungo cha maisha, watuhumiwa 14 walihukumiwa miaka 30.

ACP Masejo ameendelea kufafanua kuwa kwa kipindi kama hicho Jeshi hilo lilifanikiwa kupunguza ajali za barabarani kwa Asilimia 19 ambapo Mwaka 2022 ajali zilizoripotiwa zilikuwa 90 ukilinganisha na ajali 73 zilizoripotiwa mwaka 2023 ambapo ni sawa na upungufu wa ajali 17.

Sambamba na hilo pia kupitia misako mbalimbali walioifanya Mwaka 2023 dhidi ya Madawa ya Kulevya, walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 198 wakiwa na Mirungi Tani mbili na Kilogramu 250.7.

Pia Watuhumiwa 250 walikamatwa wakiwa na Bangi Tani Sita na Kilogramu 462.8 huku Jeshi hilo likiteketeza jumla ya hekari 70 za bangi na kukamata watuhumiwa 15 wakiwa na Heroine gramu 860.75 huku Watuhumiwa 140 walihukumiwa vifungo mbalimbali.

Halikadhalika kwa kipindi hicho Jeshi hilo lilifanikiwa kukamata Watuhumiwa 417 wakiwa na pombe ya Moshi maarufu kwa jina la gongo lita 1,338.9 pamoja na mitambo 51 ya kutengeneza pombe hiyo huku Watuhumiwa 152 wakihukumiwa vifungo mbalimbali.

Kamanda Masejo amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za wananchi, Askari wa Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya usalama pamoja na Vyombo vya Habari katika kuhabarisha na kufichua vitendo vya kihalifu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewahakikishia wananchi kuwa limejipanga vyema kuhakikisha mwaka 2024 Mkoa huo unakua shwari wakati wote, ambapo limesema kuwa halitoruhusu mtu yoyote ama kikundi cha watu kitakachojaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwani litawachukulia hatua za kisheria kwa watakaobainika hasa kwa kuzingatia Mkoa huo ni kitovu cha utalii hapa Nchini.

Share: