Zimbabwe yazindua kampeni ya nyumba kwa nyumba ya chanjo ya kipindupindu

Zimbabwe siku ya Jumatatu ilizindua kampeni ya chanjo ya kipindupindu ili kutoa chanjo ya zaidi ya watu milioni 2 dhidi ya ugonjwa unaoenezwa na maji, huku kukiwa na mlipuko ambao umeua mamia tangu mapema mwaka jana.

Kipindupindu kilikuwa kimeua watu 452 na kuambukiza jumla ya 20,446 katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kufikia Januari 24, tangu mlipuko huo uanze Februari 2023, kulingana na takwimu za wizara ya afya. Karibu nusu ya kesi zimehusisha watoto.

''Zimbabwe itapokea jumla ya dozi milioni 2.3 za chanjo kutoka kwa UNICEF na Shirika la Afya Duniani zitakazotumwa katika wilaya 29 kati ya zilizoathirika zaidi. Zaidi ya dozi 892,000 tayari zimetumwa,'' wizara ya afya ilisema. 

Kampeni ya usambazaji wa chanjo ya kipindupindu ilizinduliwa huko Kuwadzana, kitongoji kilicho umbali wa kilomita 15 kutoka katikati mwa Harare. 

Wahudumu wa afya walitoa chanjo ya kwanza kwa watoto wa shule huku kukiwa na wito kwa wakazi kushiriki. Pia wameanza kwenda nyumba kwa nyumba kutoa chanjo hiyo.

Share: