Wawili hao walikamatwa siku ya Alhamisi katika mji mkuu, Lusaka, pamoja na jamaa mwingine wa karibu aliyetambulika kama Charles Phiri
Mke wa Rais wa zamani wa Zambia Esther Lungu na bintiye Chiyeso Katete wamekamatwa kwa kumiliki mali zinazoshukiwa kuwa ni za uhalifu.
Wawili hao walikamatwa siku ya Alhamisi katika mji mkuu, Lusaka, pamoja na jamaa mwingine wa karibu aliyetambulika kama Charles Phiri, mamlaka ilisema.
Bi Lungu "alishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha" ya jinsi alivyopata shamba la $30,000 (£24,000) katika mji mkuu, shirika la kupambana na dawa za kulevya lilisema.
Rais wa zamani Edgar Lungu alisema familia hiyo itapinga mashtaka hayo mahakamani. Kiongozi huyo wa zamani amekuwa akiishutumu serikali kwa kumuonea yeye na wanachama wa chama chake cha Patriotic Front (PF) kumzuia kurejea kwenye siasa kabla ya uchaguzi wa 2026.
Hivi karibuni alidai kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa sababu ya shughuli zake za kisiasa zilizokithiri ingawa serikali ilikanusha.
Septemba mwaka jana, mkewe alikamatwa kwa tuhuma za rushwa, zinazohusisha kesi za wizi wa magari na hati miliki, tuhuma ambazo alikanusha.
Siku ya Alhamisi, Bi Lungu, 66, alikamatwa kwa tuhuma za kujipatia mali isiyohamishika ya kifahari huko Lusaka, Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DEC) ilisema katika taarifa.
Ilisema Bi Lungu anamiliki "nyumba 15 za ghorofa mbili" zilizoko katika eneo la State Lodge katika mji wa Chongwe, Lusaka, "inayoshukiwa kuwa mapato ya uhalifu".
Tarehe kamili ya mali hiyo, inayomilikiwa kwa pamoja na watu wengine wasiojulikana, haikujulikana lakini DEC ilisema ilinunuliwa kati ya 2015 na 2023.
DEC ilisema binti yake alikabiliwa na mashtaka ya ziada ya kupata shamba huko Lusaka, linaloshukiwa kununuliwa kwa njia ya ulaghai.
Wote waliachiliwa kwa dhamana, alisema Bw Lungu, akiongeza kuwa walikuwa salama nyumbani baada ya kuhojiwa na maafisa wa DEC kwa saa kadhaa siku ya Alhamisi.
Binti mwingine wa Bi Lungu, Tasila, anakabiliwa na mashtaka tofauti lakini yanayohusiana na hayo, kulingana na DEC.
Ameagizwa, kupitia mawakili wake, kufika DEC siku ya Jumatatu.
Washtakiwa hawakuzungumzia madai hayo lakini katika taarifa fupi, rais huyo wa zamani alisema familia itawapinga mahakamani.
Haijabainika mara moja ikiwa na lini watafikishwa mahakamani.
Bw.Lungu alitangaza kurejea katika siasa Oktoba mwaka jana, na kusababisha serikali kumfutia marupurupu yake ya kustaafu.