Waziri wa uingereza david lammy ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja huko gaza

Waziri wa Uingereza David Lammy ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja huko Gaza wakati wa ziara yake ya kwanza nchini Israel na maeneo ya Palestina kama waziri wa mambo ya nje.

"Niko hapa kushinikiza kusitishwa kwa mapigano," alisema. "Kupoteza maisha katika miezi michache iliyopita... ni ya kutisha. Inabidi ikome."

Bw Lammy pia alihimiza kuachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa Gaza na kuongezeka kwa misaada katika eneo hilo.

Waziri huyo mpya aliyechaguliwa alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina Mohammad Mustafa siku ya Jumapili.

Baadaye anatarajiwa kukutana na Rais wa Israel Isaac Herzog na familia za baadhi ya mateka wenye uhusiano na Uingereza.

"Ni muhimu kwamba, wakati tuko kwenye vita, vita hivyo viendeshwe kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu," Bw Lammy alisema.

"Bila shaka nitakuwa nikisisitiza viongozi wa Israel juu ya suala hilo katika siku zijazo."

Waziri huyo wa mambo ya nje pia alionyesha kufadhaika kutokana na ukosefu wa malori ya misaada ya Uingereza inayoingia Gaza "baada ya miezi na miezi ya kuomba" hilo kufanyika, akirejelea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada kuhusu kuzuiwa au kucheleweshwa kwa ukaguzi tata uliowekwa na jeshi la Israel.

Alisema hali ya kibinadamu huko Gaza ilikuwa "ya kutisha" na kwamba Uingereza itakuwa ikitoa pauni milioni 5.5 za ziada kwa shirika la matibabu la UK-Med kufadhili kazi yake katika eneo hilo.

Chama cha Labour hivi majuzi kimekabiliwa na msukosuko kutoka kwa baadhi ya wapiga kura Waislamu kuhusu jibu lake kwa mzozo huo, ambao wengi wanauona kuwa hautoshi kuikosoa Israel.

Serikali mpya sasa inakabiliwa na maamuzi juu ya masuala kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na kuweka kikomo au kusimamisha uuzaji wa silaha kwa Israel kutokana na raia kupoteza maisha.











Share: