Waziri mkuu wa israel benjamin netanyahu ameapa kukataa vikwazo vyovyote kwa jeshi la israel

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kukataa vikwazo vyovyote kwa jeshi la nchi hiyo, baada ya ripoti kuwa Marekani inapanga kupunguza msaada kwa kitengo kimoja.

"Nitapambana nayo kwa nguvu zangu zote," waziri mkuu alisema Jumapili.

Hapo awali, tovuti ya habari ya Axios ilisema Marekani italenga kikosi cha Netzah Yehuda cha Israel kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Alipoulizwa wiki iliyopita kuhusu ripoti kwamba msaada wa kijeshi wa Marekani kwa vitengo vya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) unaweza kupunguzwa kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alisema: "Nimefanya maamuzi; unaweza kutarajia kushuhidia katika siku zijazo".

Marekani - mshirika mkuu wa Israel - haijawahi kusimamisha msaada kwa kitengo cha IDF siku za nyuma.

Jeshi la Israel lilisema Netzah Yehuda ilikuwa inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

"Kufuatia machapisho kuhusu vikwazo dhidi ya kikosi hicho, IDF haifahamu suala hilo," jeshi limenukuliwa likisema na shirika la habari la Reuters. "IDF inafanya kazi na itaendelea kufanya kazi kuchunguza tukio lolote lisilo la kawaida kwa njia ya vitendo na kwa mujibu wa sheria."

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant aliitaka Marekani kuondoa nia yake ya kuiwekea vikwazo Netzah Yehuda, akisema dunia inaangalia uhusiano kati ya Marekani na Israel kwa karibu zaidi kuliko hapo awali.

"Jaribio lolote la kukosoa kitengo kizima linasababisha kufuatiliwa kwa karibu vitendo vya IDF," taarifa kutoka kwa Bw Gallant ilisema, na kuongeza "hii sio njia sahihi kwa washirika na marafiki".










Share: