Vyombo kadhaa vya habari viliripoti kuhusu ziara ya Bw Orban, vikinukuu vyanzo vyao.
Viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya wameelezea wasiwasi wao kuhusu ripoti za vyombo vya habari kwamba Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban huenda atakutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow siku ya Ijumaa.
Bw Orban - ambaye nchi yake sasa inashikilia urais wa zamu wa EU - ndiye mkuu pekee wa serikali ya kitaifa ya umoja huo kuwa na uhusiano wa karibu na Kremlin kufuatia uvamizi wake Ukraine mnamo 2022.
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel alisema Bw Orban "hakuwa na mamlaka ya kuwasiliana na Urusi kwa niaba ya EU", huku Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk akiomba ufafanuzi.
Vyombo kadhaa vya habari viliripoti kuhusu ziara ya Bw Orban, vikinukuu vyanzo vyao.
Gazeti la Financial Times lilisema maafisa mmoja wa Hungary na wawili wa Umoja wa Ulaya wamethibitisha ripoti za vyombo vya habari kwamba Bw Orban atakutana na rais wa Urusi siku ya Ijumaa.
Radio Free Europe/Radio Liberty, shirika la vyombo vya habari linalofadhiliwa na serikali ya Marekani, lilinukuu chanzo cha serikali ya Hungary.
Pia ilisema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary Peter Szijjarto ataandamana na Bw Orban.
Hungary na Urusi hazikujibu ombi la BBC la kuthibitisha ripoti hizo.
Mnamo Jumatatu, kulingana na shirika la habari la AFP, Bw Orban aliahidi "habari za kushangaza kutoka sehemu za kushangaza".