Waziri makamba apokea nakala za hati za utambulisho za balozi mteule wa libya nchini

Ni faraja kwangu kuja kufanya kazi Tanzania naahidi wakati wote wa uwakilishi wangu hapa Tanzania kama Balozi tutafanya kazi kwa ushirikiano katika kuendeleza sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, kilimo na nyingine.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makamba amemkaribisha nchini Mhe. Alshatewi na kumuahidi ushirikiano wa Wizara na Serikali kwa ujumla wakati wote atakaokuwa akitekeleza majukumu yake nchini.

Aidha, Waziri Makamba ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Libya umedumu kwa zaidi ya miaka 50 na na wakati wote umekuwa imara. “Tunaamini kuwa Mhe. Balozi wakati wa uwakilishi wako uhusiano baina ya mataifa yetu utaendelea kuimarika zaidi katika sekta mbalimbali za kimkakati,” aliongeza Waziri Makamba.

Kwa upande wake Balozi Mteule, wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi amesema kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na Tanzania wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi hapa nchini.

Ni faraja kwangu kuja kufanya kazi Tanzania naahidi wakati wote wa uwakilishi wangu hapa Tanzania kama Balozi tutafanya kazi kwa ushirikiano katika kuendeleza sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, kilimo na nyingine.

Katika tukio jingine, Waziri Makamba amekutana kwa Mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot, Balozi wa Vatican nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino pamoja na Naibu Balozi wa Marekani nchini, Bw. Robert Raines.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Makamba amejadiliana na Mabalozi hao masuala mbalimbali ya ushirikiano wa uwili, kikanda na ushirikiano wa kimataifa baina ya Tanzania na nchi zao.

Share: