Waziri dkt. gwajima ataka usawa wa kijinsia eneo la uchumi kutiliwa mkazo.

Waratibu wa Programu ya Jukwaa la kizazi chenye usawa wametakiwa kutambua masuala yaliyowekewa Ahadi hususan upande wa kiuchumi ambapo Tanzania ni kinara wa eneo hilo kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa maelekezo hayo Januari 15, 2024 wakati akifungua mafunzo ya Programu hiyo kwa waratibu wa ngazi za mikoa na Halmashauri yanayofanyika kwa siku mbili mkoani Mwanza na kukamilisha mafunzo kwa mikoa yote 26 na halmashauri 184 nchini.

Waziri Dkt. Gwajima amewaagiza waratibu hao kuratibu Afua zinazotekelezwa na sekta zao na kuzitolea taarifa kwa wakati pamoja na kutambua wadau waliopo na afua wanazotekeleza.

Amefafanua kuwa, haki hizo zinatakiwa kuwa na sura ya usawa wa kijinsia kwamba siyo tu wanaume wanufaike zaidi na fursa za kiuchumi bali wanawake pia wanufaike kwa kwani, takwimu zinaonesha kuwa wamekuwa nyuma ikilinganishwa na wanaume hivyo kuathiri mfumo mzima wa nafasi yao kwenye kusukuma maendeleo na ustawi wa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hasan Masala amesema mkoa huo umefanya kazi kubwa ya masuala ya usawa wa kijinsia kutokana na utashi wa Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jinsia na Wanawake Juliana Kibonde amesema waratibu hao wana jukumu la kuhakikisha kunakuwa na mlengo wa kijinsia katika miradi, afua na masuala ya uongozi kwenye maeneo yao Ili kufikia usawa kwenye hilo eneo haki na usawa wa kiuchumi.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Linus Kahendaguza amesema mafunzo hayo ni ya awamu ya pili kwa Mikoa 15, ambapo awamu ya kwanza yalifanyika kwa mikoa 11 mkoani Dar Es Salaam.

Mafunzo hayo yanatokana na Ahadi za nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye usawa ambalo chimbuko lake ni tathmini ya utekelezaji wa Azimio la Beijing iliyoonesha kuna haja ya kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wa malengo ya Usawa wa Jinsia kwenye maendeleo ya kisekta. Serikali ya Tanzania ilichagua eneo la Haki na Usawa wa Kiuchumi na kuandaa mpango wa utekelezaji ambao ni Programu ya Kizazi Chenye Usawa Tanzania kwa kipindi cha Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) ili kufikia Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.

Share: