Ili mitaala itekelezwe kwa ufanisi ni lazima kuwe na walimu wenye weledi katika ufundishaji.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Tecknolojia, Dk Franklin Rwezimula amewataka wawezeshaji kitaifa wa mtaala wa Elimu ya Awali nchini kuzingatia mafunzo kwa umakini ili kuwawezesha walimu kutekeleza mtaala huo kwa weledi, kwani mtaala unaotarajia kuanza mwaka 2024 kwa ngazi ya elimu ya awali na msingi.
Ameyasema hayo leo tarehe 13/11/2023 alipofungua mafunzo kwa wawezeshaji hao ambao watakwenda kutoa mafunzo kwa walimu wengine nchini katika kutekeleza mtaala mpya.
“Ili mitaala itekelezwe kwa ufanisi ni lazima kuwe na walimu wenye weledi katika ufundishaji, naomba sana wawezeshaji mzingatie haya mafunzo mnayopatiwa hapa ili muweze kuifanya kazi yenu ya uwezeshaji vyema” amesema, Dkt. Rwezimula.
Ameongeza kwa kusema kuwa Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha mafunzo endelevu kazini ili kuhakikisha walimu wanakuwa bora katika maeneo yao ya kazi. ikiwemo uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa kuboresha miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo vifaa vya TEHAMA.
Katika hatua nyingine, Dkt. Rwezimula ameipongeza TET kwa usimamizi mzuri wa mitaala huku akioongeza kuwa mabadiliko ya mtaala yaliyofanyika yataanzia katika ngazi ya Darasa Awali, darasa la kwanza na darasa la tatu; kwa kuanzia na kusema serikali imejipanga katika kuhakikisha mtaala huo unatekelezwa vyema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema kuwa Mitaala imefanyiwa maboresho ambayo ni makubwa na ya sita tangu nchi yetu ipate uhuru.
"Tumeboresha muundo wa elimu na sasa elimu ya awali itatolewa kwa muda wa mwaka mmoja kwa watoto wenye umri wa miaka mitano ambapo elimu ya awali itatanguliwa na elimu ya malezi na makuzi itakayotolewa kwa miaka miwili kwa watoto wenye umri wa miaka mitatu mpaka minne, elimu hii itasimamiwa na wizara inayosimamia ustawi wa watoto ambayo kwa sasa ni wizara ya maendeleo ya jamii jinsia ,wanawake na makundi maalumu “amesema Dkt. Komba.
Ameongeza kwa kusema kuwa yapo maboresho yaliyofanywa kwenye maeneo ya ujifunzaji ambapo kwa sasa mtaala una maeneo makuu matano ambayo ni 1. Utamaduni, elimu ya imani, sanaa na michezo. 2. Lugha na mawasiliano 3. Stadi za awali za maisha. 4 Afya na mazingira 5.Stadi za awali za kihisabati, kisayansi na TEHAMA.
Mafunzo hayo yatafanyika katika maeneo mbalimbali , ambapo awamu ya kwanza yameanza kufanyika Mkoani Iringa na baadae kufanyika katika mikoa ya Mwanza na Dar es salaam, ambapo yanaratibiwa na TET kupitia mradi wa GPE LANES II ambao utahusisha waratibu wawezeshaji wa kitaifa ambao watapeleka ujuzi wao kwa walimu wengine nchi nzima.