Wilbard John Chambulo Amedai kuwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamekuwa wakitengeneza nyaraka bandia
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Arusha kuanza uchunguzi dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Injinia Juma Hamsini na baadhi ya wasaidizi wake kutokana na kukabiliwa na tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa fedha za walipa kodi.
Akizungumza na wadau wa utalii Mkoani Arusha leo Jumamosi Mei 18, 2024, Mhe. Paul Christian Makonda amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Missaile Mussa kuwasimamisha kazi watumishi wote waliotajwa kuhusika na tuhuma hizo ili kupisha uchunguzi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amechukua hatua hizo baada ya Mwenyekiti wa waongoza watalii mkoa wa Arusha Wilbard John Chambulo kudai kuwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamekuwa wakitengeneza nyaraka bandia pamoja na kuchepusha baadhi ya makusanyo ya kodi zinazotokana na sekta ya Utalii.
Chambulo amemuambia Mkuu wa Mkoa kwamba Watumishi hao wamekuwa na makampuni hewa ya utalii pamoja na kuwa na namba tofauti za ulipaji wa kodi na usajili hewa wa makampuni yenye kufanana na makampuni halisi ya utalii yalipo ndani ya Jiji la Arusha.
Mara baada ya malalamiko hayo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema serikali yake inawajibikaji kuwa mlezi wa wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa wa Arusha na hivyo kamwe hatovumilia mtendaji yeyote anayekuwa sababu ya kukua kwa vitendo vya rushwa na kuua biashara zilizopo mkoani Arusha.
Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku kwa Halmashauri zilizopo mkoani Arusha kutumia Polisi kwenda kudai kodi kwa wafanyabiashara na kuagiza zitumike teknolojia zaidi kwenye kukumbusha na kudai madai mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Arusha.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda amelazimika kuahirisha kikao kazi hicho na kuagiza kupangwa kwa tarehe nyingine chini ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha ili kupata muda mzuri wa kujadiliana na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazokwamisha ukuaji na ustawi wa sekta ya Utalii mkoani Arusha.