Wapinzani wa libya wakubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa

Viongozi wa serikali mbili zinazohasimiana nchini Libya wamekubaliana kuunda serikali muungano wa kitaifa, jambo linaloashiria hatua iliyopigwa katika juhudi za kumaliza mkwamo wa kisiasa ambao umedumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Katika taarifa ya pamoja siku ya Jumapili, viongozi hao walisema wamekubaliana juu ya "umuhimu" wa kuunda serikali mpya ya umoja ambayo itasimamia uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu na "kuunganisha nyadhifa kuu".

Mazungumzo hayo yalifanyika katika mji mkuu wa Misri, Cairo, na yaliongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmed Aboul Gheit.

Mazungumzo hayo yaliwahusisha rais wa Baraza la Rais wa Libya na mkuu wa Baraza Kuu la Serikali, wote wenye makao yake mjini Tripoli, pamoja na spika wa Baraza la Wawakilishi katika utawala hasimu wenye makao yake makuu mjini Benghazi.

Libya ilianza kuvunjika baada ya kuanguka kwa mtawala wa muda mrefu Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Nchi hiyo imegawanyika kati ya serikali inayotambulika kimataifa upande wa magharibi, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa mpito Abdul Hamid Dbeibah mjini Tripoli, na utawala wa mashariki unaoendeshwa na mwanajeshi Khalifa Haftar mjini Benghazi.

Share: