Makamu wa Rais anaendelea na Ziara mkoani Kigoma yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaagiza Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi kwa ujumla kutumia magari wanayokabidhiwa kwa kufanya kazi za wananchi ikiwemo kuwatembelea na kutatua changamoto zinazowakabili.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikabidhi magari matano kwa Wakuu wa Wilaya Tano za Mkoa wa Kigoma akiwa ziarani mkoani humo. Amesema bado utekelezaji wa agizo lililotolewa kwa viongozi kuwatembelea wananchi katika maeneo yao halitekelezwi kikamilifu.
Aidha amewasihi viongozi hao kutunza magari na kuyatumia kwa matumizi sahihi ikiwemo kufuata maadili ya utumishi wa umma. Ameagiza magari hayo kutotumika vibaya na kuonekana katika maeneo ya starehe. Amesema magari hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuwatembelea wananchi kwa kasi zaidi.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Mwana Anthropolojia na Mwana Primatolojia aliyetafiti kuhusu Maisha ya Sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe mkoani Kigoma Bi. Jane Goodall, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ndogo Kigoma.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amempongeza na kumshukuru Bi. Goodall kwa mchango wake katika uhifadhi hapa nchini na kuitangaza Hifadhi ya Gombe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
Akizungumza na Wananchi wa Kigoma wakati akifungua barabara iliyopewa jina la mtafiti Bi. Jane Goodall inayoelekea eneo la kibirizi ziwani kwenda Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Makamu wa Rais amesema Bi. Goodall ametoa mchango mkubwa katika kutoa elimu ya viumbe na mwalimu muhimu wa uhifadhi.
Amewahimiza vijana na kuwasisitiza kujifunza zaidi elimu ya hifadhi ya misitu na mazingira kwa ujumla. Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kutambua mchango wa Mtafiti huyo na kuweka alama ya barabara itakayokumbuka mchango wake.
Makamu wa Rais anaendelea na Ziara mkoani Kigoma yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi.