Wakenya wapata likizo ya kupanda miti ili kupanda miche milioni 100

Wakenya wamepewa likizo maalum ya kupanda miti milioni 100 kama sehemu ya lengo la serikali kupanda miti bilioni 15 katika kipindi cha miaka 10.

Likizo hiyo inaruhusu "kila Mkenya kumiliki mpango huo", kulingana na Waziri wa Mazingira Soipan Tuya.

Kila Mkenya anahimizwa kupanda angalau miche miwili, hivyo basi kufikia lengo la milioni 100.

Takriban miche milioni 150 imepatikana katika vitalu vya umma.

Serikali itakuwa ikitoa miche hiyo bila malipo katika vituo vya wakala wa misitu ili Wakenya waipande katika maeneo maalum ya umma.

Lakini pia imewahimiza Wakenya kununua angalau miche miwili ili kuipanda katika ardhi yao wenyewe.

Rais William Ruto anaongoza zoezi hilo eneo la Makueni mashariki mwa nchi. Mawaziri wametumwa katika mikoa mingine kuongoza shughuli hiyo pamoja na magavana wa kaunti.

Upandaji miti utafuatiliwa kupitia programu (app) ya mtandao, ambayo inafuatilia zoezi hilo kwa kuruhusu watu binafsi na mashirika kurekodi shughuli, ikiwa ni pamoja na aina ya mimea, nambari na tarehe iliyopandwa.

Programu ya Jaza Miti pia itasaidia watu kupanda miche inayofaa kwa kulinganisha eneo la ardhi na spishi zinazofaa, kulingana na wizara ya mazingira.

Bi Tuya aliaambia televisheni ya Citizen nchini humo siku ya Jumapili usiku kwamba muitikio uilikuwa "wa kushangaza" na tayari kulikuwa na usajili milioni mbili kwenye programu kufikia Jumapili.

Hata hivyo alisema upandani wa miche hiyo hautafanyika katika eneo la kaskazini-mashariki, ambako kumekuwa na mafuriko.

Share: