Waganga wakuu wa mikoa na halmashauri simamieni huduma za matibabu ya meno kabla ya kufikia kung’oa

Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wametakiwa kuhakikisha wanasimamia matibabu bora ya Kinywa na Meno na kupunguza kung’oa meno bali waongeze watu wanaotibiwa meno.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Novemba 22, 2023 wakati akifungua Kongamano la 38 la kisayansi la Kitaifa na mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno linalofanyika Jijini Tanga. 

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Takwimu za kuziba meno zimeongezeka kutoka asilimia 2 mwaka 2020 mpaka asilimia 36.1 mwaka 2023 ambapo hali hii imetokana na uwekezaji wa Serikali ya awamu Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. 

Pia, Waziri Ummy amesema katika jitihada za Serikali za kuendelea kufanya mapinduzi Katika Sekta ya Afya imeweza kuajiri wataalam wa Kinywa na Meno 186 na kununua vifaa tiba vya kinywa na meno ikiwemo viti vya kutibia 55 vilivyokwenda kwenye Halmashauri 40 katika Mikoa yote nchini. 

Amesema, Mwaka 2023/24 katika robo ya Kwanza na ya Pili ya mwaka jumla ya viti 207 vimeenda kwenye Halmashauri 160 vifaa tiba vya uchunguzi 82 zimeenda kwenye Halmashauri 70, na OPG mashine 1, CBCT mashine 1, gharama za Vitu vyote hivi ni zaidi ya TZS. Bilioni Saba.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema Sambamba na uwekezaji huo, Serikali imeongeza ufadhili wa wataalam wa Sekta ya Afya hasa nafasi za kibingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi kwa kutenga shilingi bilioni 8 ambapo kati ya hizo Tsh. Bil 3 zimetengwa kwa ajili ya kusomesha wataalamu kwa seti ili kuleta ufanisi wakati wa utoaji huduma za kibingwa bobezi za Afya.

Share: