Waandamanaji wa israel wamezuia malori yanayopeleka misaada gaza

Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zinaielezea kama kundi la mrengo wa kulia ambalo linatafuta kusitisha uhamishaji wa misaada ya kibinadamu hadi Gaza

Waandamanaji wa Israel wamezuia malori ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza siku ya Jumatatu, wakitupa vifurushi vya chakula barabarani na kufungua magunia ya nafaka katika eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi.

Malori hayo, ambayo yaliwekwa kwenye kizuizi cha Tarqumiya magharibi mwa Hebroni, yalitoka Jordan na yalikuwa yakielekea Ukanda wa Gaza, ambapo makumi ya maelfu ya Wapalestina wanakabiliwa na uhaba wa chakula na misaada.

Ikulu ya White House imelaani shambulizi hilo, ikilemea "uporaji" wa misafara ya misaada.


Kundi linaloripotiwa kuwa kwenye maandamano hayo lilisema walikuwa wakiandamana kupinga kuendelea kuzuiliwa kwa mateka wa Israel huko Gaza.

Picha ambazo hazijathibitishwa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha waandamanaji wakiangusha masanduku kutoka kwenye lori na kuyakanyaga mara yalipoanguka.

Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Israel, kundi la wanaharakati la Tzav 9 lilihusika kuandaa maandamano hayo.

Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zinaielezea kama kundi la mrengo wa kulia ambalo linatafuta kusitisha uhamishaji wa misaada ya kibinadamu hadi Gaza huku mateka wa Israel wakishikiliwa huko.

Muandamanaji mmoja aliliambia shirika la habari la AFP kuwa alikuwa katika kituo cha ukaguzi siku ya Jumatatu kwa sababu alisikia malori ya misaada yalikuwa "yakielekea mikononi mwa Hamas, ambao wanajaribu kuwaua wanajeshi wengine na raia wengine wa Israel".

Hana Giat, mwenye umri wa miaka 33, alisema "hakuna chakula kinachopaswa kuingia Gaza" hadi mateka wa Israeli warudishwe "wakiwa hai na wenye afya".

Katika taarifa iliyonukuliwa na gazeti la Jerusalem Post, Tzav 9 ilikataa baadhi ya vitendo vya waandamanaji, ikisema kuwa "vitendo vilivyofanywa haviendani na maadili ya harakati zetu."

Iliongeza, hata hivyo, kwamba "kuzuia malori ni hatua ya ufanisi na ya vitendo ambapo tunapiga kelele kwamba 'hakuna msaada unaopita hadi mateka wa mwisho arudi'".

Waandamanaji wanne, akiwemo mtoto mdogo, walikamatwa kwenye maandamano hayo, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mawakili wao.

Share: