Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema majaribio yanayofanyika sasa yanahusisha vichwa vya treni
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaaga Viongozi wa Dini 104 na Watu wengine mbalimbali ambao wamesafiri na treni ya mwendokasi ambayo imefanya safari yake ya kwanza ya majaribio April 21,2024 kutoka Dar es salaam kuelekea Dodoma ambako wamekwenda kushiriki Ibada maalum ya kuliombea Taifa inayotarajiwa kufanyika Jumatatu April 22,2024.
Treni hiyo imeondoka stesheni ya Dar es Salaam leo ikiwa na Viongozi wa Dini, Waandishi wa Habari, Waimbaji wa nyimbo za injili na kaswida, Viongozi Wastaafu wa Serikali, Watendaji wa Shirika la Reli, Wawakilishi wa Ubalozi na Watendaji wengine wa Serikali
PM Majaliwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuleta maendeleo na hasa kuboresha miundombinu kwenye maeneo mengi ikiwemo reli, maji, usafiri wa anga, na barabara.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema majaribio yanayofanyika sasa yanahusisha vichwa vya treni, mabehewa na mifumo ya umeme “Hii ni mara ya kwanza tunaenda Dodoma, lakini tumejipanga ili ifikapo July mwaka huu usafiri wa treni ya abiria kutokea Dar hadi Dodoma uwe umeanza kama Mheshimiwa Rais Samia alivyoagiza”