Ukraine Muagizaji mkubwa zaidi wa silaha duniani - Sipri

Ripoti mpya iliyochapishwa leo Jumatatu na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) inasema nchi za Ulaya zilizomo kwenye Jumuiya ya NATO ziliongeza zaidi ya maradufu uagizaji wa silaha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku ikinunua zaidi ya asilimia 60 ya silaha kutoka nchini Marekani.

Matokeo haya ya SIPRI yanakwenda sambamba na tangazo la Umoja wa Ulaya kwamba wanakusudia kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa bara hilo ili kukabiliana na mabadiliko ya sera za kigeni za Marekani chini ya Rais Donald Trump.

Ripoti hiyo inaitaja Ukraine kuwa muagizaji mkubwa zaidi wa silaha duniani katika kipindi cha 2020 hadi 2024.

Marekani ilisalia kama muuzaji mkubwa wa silaha duniani, kwa mauzo ya nje yaliyofikia asilimia 43, ikifuatiwa na Ufaransa, iliyouza kwa asilimia 9.6.

Manunuzi ya silaha yaliyofanywa na nchi wanachama wa NATO barani Ulaya yaliongezeka kwa asilimia 105, ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita, na kulingana na Mkuu wa programu ya Mauzo ya Silaha kwenye taasisi hiyo Mathew George, hii inaashiria maandalizi ya mataifa hayo katika kukabiliana na kitisho cha Urusi lakini pia kutokuwa na uhakika juu ya mwelekeo wa baadaye wa sera ya kigeni ya Marekani.

Kulingana na ripoti hiyo, nchi 35 zilipeleka silaha nchini Ukraine katika kipindi cha kati ya 2020 na 2024, huku Marekani ikipeleka asilimia 45 ya silaha, ikifuatiwa na Ujerumani kwa asilimia 12 na Poland asilimia 11. Urusi bado ni nchi ya tatu kwa mauzo ya silaha, licha ya kupungua kwa asilimia 64 ya mauzo ya nje katika kipindi cha 2020-24 ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.

Share: