Taarifa iliyotolewa na serikali imesema ufunguzi wa ofisi hiyo unaashiria hatua muhimu katika uhusiano
Uingereza imekuwa miongoni mwa mataifa machache ya Ulaya kufungua ofisi ndogo ya ubalozi jijini Dodoma ambayo ni makao makuu ya Tanzania.
Nchi hiyo imefuata nyayo za Ujerumani na Ufaransa kwa upande wa Ulaya, China kwa bara Asia na Umoja wa Mataifa waliofungua ofisi awali.
Taarifa iliyotolewa na serikali imesema ufunguzi wa ofisi hiyo unaashiria hatua muhimu katika uhusiano kati ya Uingereza na Tanzania.
Imesema kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uwepo mjini Dodoma, ofisi hii itawezesha kufanya kazi kwa ukaribu kati ya serikali ya Uingereza na Tanzania na pia wadau wengi kutoka nchi zote mbili. Kwenye uzinduzi huu, Waziri Mitchell aliungana na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba na balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar.
"Ni heshima kubwa kufungua ofisi mpya ya Serikali ya Uingereza nchini Tanzania. Haswa ni heshima ya pekee kufungua ofisi hii mjini Dodoma katika mwezi ambao Tanzania inasherehekea miaka 60 ya Muungano.
Siku ya leo ni ishara ya imani na thamani tunayoweka katika ushirikiano wetu na Serikali ya Tanzania. Pia ni matokeo ya uhusiano muhimu na wa kudumu kati ya watu wa mataifa mawili yenye ushirikiano na urafiki katika ngazi zote." Alisema Waziri Mitchell.
Katika ziara yake ya siku mbili nchini Tanzania, waziri Mitchell alihudhuria mikutanombalimbali ya ngazi ya juu mjini Dodoma na Dar es Salaam ikiwemo kukutana na waziri wa Uwekezaji na Mipango, KitilaMkumbo.
Jijini Dar es Salaam, Waziri Mitchell alitembelea kliniki ya afya ili kujionea jinsi gani ongezeka la ufadhili wa dola milioni 15 kupitia serikali ya Uingereza itaendelea kusaidia Tanzania katika huduma za uzazi wa mpango.
Waziri pia alitembelea kikosi kazi cha kupambana na usafirishaji haramu wa Binadamu na Ulinzi wa watoto pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dr. Seif Shekalaghe.
Kikosi Kazi kinachofadhiliwa na serikali ya Uingereza kinafanyia majaribio ya mbinu mpya za kukabiliana na biashara haramu ya binadamu na unyanyasaji wa kingono kwa watoto.