
Uingereza na washirika wake wako tayari kuunga mkono Ukraine kabla ya mazungumzo ya kumaliza vita na hatimaye kufikia makubaliano ya amani, waziri wa ulinzi wa Uingereza anasema.
Katika mkesha wa mkutano wa ngazi ya juu mjini Paris, John Healey aliiambia BBC mjini Kyiv kwamba washirika wa Ukraine "watasaidia kufanya anga, bahari kuwa salama, na kulinda ardhi", mara tu makubaliano ya amani yatakapofikiwa.
Lakini muda mfupi kabla ya hapo, Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa amewasilisha ujumbe wa dharura kutoka China, akiapa kwamba uvamizi wake kamili unaweza kuendelea.
Healey alipendekeza kwamba kulikuwa na vitisho katika maneno ya Putin, akisisitiza kuwa Urusi ilikuwa chini ya shinikizo.
Pia alimsifu Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alisema "alimleta Putin kwenye mazungumzo" na bado "hajashikilia msimamo wowote", licha ya ukosoaji mkubwa wa makaribisho mazuri ambayo Trump alimpa kiongozi huyo wa Urusi mwezi uliopita huko Alaska.
Alipoulizwa Jumatano ikiwa vita vya Ukraine vinaweza kumalizika hivi karibuni, Putin alisema "kuna matumaini ya kufaulu".
"Kwangu ninaona busara ikitawala, kuna uwezekano wa kukubaliana juu ya suluhu la kumaliza mzozo huu," alisema, kabla ya kutishia: "Ikiwa sivyo, basi itabidi kutatua tuliyonayo kijeshi."