UFARANSA YALITAMBUA RASMI TAIFA LA PALESTINA

Ufaransa imelitambua rasmi taifa la Palestina, na kuwa nchi ya hivi punde zaidi katika wimbi la nchi kuchukua hatua hiyo.

Akizungumza katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Emmanuel Macron alisema "wakati wa amani umefika" na kwamba "hakuna kinachohalalisha vita vinavyoendelea Gaza".


Ufaransa na Saudi Arabia zinaandaa mkutano wa siku moja katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoangazia mipango ya suluhu la mataifa mawili katika mzozo huo. Mataifa ya G7 Ujerumani, Italia na Marekani hawakuhudhuria.


Ubelgiji, Luxembourg, Malta, Andorra na San Marino pia zinatarajiwa kulitambua taifa la Palestina, baada ya Uingereza, Canada, Australia na Ureno kutangaza kulitambua Jumapili.


Shinikizo la kimataifa linaongezeka kwa Israeli juu ya mgogoro wa kibinadamu unaoendelea huko Gaza na ujenzi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi.


Israel imesema kutambuliwa kwake ni zawadi kwa Hamas kwa shambulio la kundi la wapiganaji la Palestina la tarehe 7 Oktoba 2023 kusini mwa Israel ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na 251 kuchukuliwa mateka.


Zaidi ya Wapalestina 65,000 wameuawa na Israel tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas. Vikosi vya Israel kwa sasa vinafanya mashambulizi ya ardhini yenye lengo la kuudhibiti mji wa Gaza, ambako watu milioni moja walikuwa wakiishi na njaa ilithibitishwa mwezi uliopita.


Kiongozi huyo wa Ufaransa aliuambia mkutano huo kuwa wakati umefika wa kusitisha vita na kuwakomboa mateka waliosalia wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas. Alionya dhidi ya "hatari ya vita visivyoisha" na kusema "haki lazima itashinda nguvu kila wakati".

Share: